Nyota wa filamu za Kihindi, Priyanka Chopra amefunguka sababu za kuacha kuigiza filamu za Bollywood na kugeukia Marekani (Hollwood).
Katika mahojiano ya hivi karibuni, Priyanka alisema sio kwamba ameacha moja kwa moja kufanya kazi za Bollywood akidai ni sehemu iliyompa umaarufu mkubwa duniani.
"Sijaacha kabisa lakini kwa sasa ni kama nina upepo mzuri na Marekani wameweka ofa nzuri ndio maana nacheza hivyo siwezi kusema moja kwa moja nimeacha," alisema Priyanka.
Aliongeza, ujasiri kumemsaidia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuaminika na kupewa dili za kuigiza Marekani ambako anaishi kwa sasa baada ya kuolewa na mwanamuziki, Nick Jonas wa kundi la Jonas Brothers.
Wawili hao walifunga ndoa mwaka 2018 kwa sherehe mbili, moja ya Kihindu na nyingine ya Kikatoliki, zikifanywa sherehe ya kawaida iliyowahusisha familia na marafiki wa karibu.
"Kama unajiambia maneno fulani ili ujisikie hodari zaidi, hiyo ni kawaida kabisa sote tunafanya hivyo, Unaweza kujiambia kuwa una nguvu zaidi ya ule ulionao kweli, ili ujisikie kujiamini mimi nimefanya hivyo mara nyingi kwenye kazi yangu,” alisema kisura huyo na kuongeza;
"Ni sawa kujijengea kujiamini mwenyewe, lakini usiwadharau au udanganye wengine. Usijaribu kuonyesha sura isiyo ya kweli wewe mwenyewe ili kupata faida kila mtu ana makosa, hiyo ni kawaida. Mie ni jumla ya makosa niliyoyafanya, bado najivunia jinsi nilivyo kufika hapa nilipo leo."
Baadhi ya filamu zilizompa umaarufu akiwa Bollywood ni Aitraaz, Fashion, Barfi, Dil Dhadakne Do, Mary Kom, na Bajirao Mastani, ilihali kwa zile za Kiingereza amefanya The Bluff, Citadel, Heads of State, Love Again, na Quantico wakati filamu ya mwisho ya Kihindi ilikuwa The Sky is Pink ya mwaka 2019.
Katika filamu mpya The Bluff, Priyanka anacheza kama Ercell Bloody Mary Bodden, mwizi wa zamani aliyeishi kwa amani visiwa vya Cayman Islands, lakini historia yake yenye ghasia inamrudisha kwenye maisha ya hatari.
Chanzo; Mwanaspoti