Wakati tabia ya mastaa wanaochipukia kuwaanika wapenzi wao kwenye mitandao ya kijamii ikishamiri, msanii wa Bongofleva, Jay Melody amesema hataweza kumtangaza mchumba wake hata iweje.
Jay Melody ambaye kwa kipindi chote cha ustaa wake hajawahi kusikika akimtaja mpenzi wake yeyote hadharani, ametaja namna mbili za mashabiki wake na jamii kumjua mpenzi wake.
Msanii huyo anayetamba na nyimbo kama Jirani, Nakupenda, Sina na Mbali Nawe, ameliambia Mwananchi kuwa waliotega masikio kumjua mpenzi wake, wasubiri siku atakapofunga pingu za maisha au akifa.
Jay Melody amesema kwa kipindi kirefu amekuwa akishindwa kutangaza uhusiano wake wa kimapenzi kwa kuhofia kuchafuliwa jina lake. Lakini kubwa zaidi hajawahi kuanzisha urafiki na wanawake wengi kama ilivyo kwa mastaa wengine.
“Uhusiano wa kimapenzi utabaki kuwa wa Jay Melody, lakini nyimbo ni zetu sote. Mpaka nitakapokufa au nitakapofunga ndoa ndipo watu watamjua mpenzi wangu ni nani. Mimi ni binadamu kama walivyo wengine, nitakuwa tayari kumtangaza mwenyewe nitakapofunga ndoa,” amesema kwa msisitizo.
Alipoulizwa uhusiano kuhusu nyimbo anazoimba zinazoonyesha dhahiri kutendwa kimapenzi, iwapo zinaendana na uhusiano wake, Jay Melody alifafanua kuwa nyimbo za aina hiyo ni sehemu ya kazi yake.
Amesema yeye alichagua kuimba aina hiyo ya muziki ili kuisemea jamii kubwa ambayo inatendwa na mapenzi.
Aidha, staa huyo amekanusha picha ya mwanadada ambaye aliwahi kuituma kwenye akaunti yake ya Instagram, ikionyesha wanajivinjari katika mbuga za wanyama na kusema ile ilikuwa ni picha ya wimbo wa ‘Nakupenda‘.
“Nakumbuka hiyo posti, ila Ile ilikuwa ni kipande cha video ya wimbo wa ‘Nakupenda,’ ndio maana kulikuwa na uwepo wa mahadhi ya mapenzi huku tukiwa karibu na mbuni na nyingine kuwalisha pundamilia huku tukibasamu,“ amesema.
Chanzo; Mwananchi Scoop