Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation, Doris Mollel amesema Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, anatarajia kuja Nchini Tanzania na kuzindua jengo maalum la kwanza Nchini kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Watoto njiti) lililopo katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza.
Doris ameyasema hayo leo February 20,2026 wakati akiongea na Waandishi wa Habari katika Ofisi za Taasisi hiyo Jijini Dar es salaam ambapo amesema jengo hilo lenye thamani ya Tsh. Bilioni 2.125 limejengwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Msanii maarufu wa Marekani Alicia Keys na kwamba tarehe ya ujio wa Dkt. Tedros na Taasisi ya Alicia Keys pamoja na tarehe ya uzinduzi zitatangazwa hivi karibuni.
Doris amesema “Nilikutana na Dkt. Tedros zaidi ya mara moja na nikamwambia tuna changamoto kubwa ya kuboresha huduma za Watoto njiti Duniani hususani Africa na nikamueleza natamani angekuja Tanzania kwa ajili ya kuzindua jengo maalum la kwanza kwa ajili ya Watoto njiti Tanzania”
“Jengo hili ni maalum kwakuwa linaenda kuhamasisha zero separation (Mtoto kutotengwa na Mama yake), Taasisi yetu imeshirikiana na Taasisi ya Msanii wa Marekani Alicia Keys ambaye ametoa mchango mkubwa kuhakikisha jengo hili linakamilika, tunaishukuru WHO wametupa mchango na hivi tunapozungumza Watumishi wapya wapo wanapewa mafunzo ya kuhakikisha huduma inakuwa bora, tunategemea pia Taasisi ya Alicia Keys kuja”
“Jengo hili lina uwezo wa kuhudumia Watoto 42 kwa wakati mmoja, unaweza kuona ni wachache ila ni kwakuwa Mama mmoja anahitaji kuwa na nafasi kubwa ili kumpa Mtoto huduma bora, lina sehemu ya Baba kuja kumuona Mama na Mtoto na hata kumlea Mtoto na tunaenda kuwapendelea Wauguzi wanaofanya kazi kwenye wodi za Watoto hawa kwakuwa tumeweka nyumba zao”
Chanzo; Millard Ayo