Akiwa na miaka takribani minane tangu ametoka kisanii, muziki wa Marioo unaendelea kuwafikia mashabiki wapya kila siku, huku akitoa kazi zenye ubora, video kali na ujumbe unaoendana na maisha ya vijana wengi.
Staa huyu mwenye albamu mbili, The Kid You Know (2022) na The God Son (2024), ni mmoja wa wasanii wa kizazi kipya walioleta ladha mpya kwenye muziki wa Bongofleva kupitia midundo ya Amapiano. Fahamu zaidi.
1. Abbah ndiye mtayarishaji muziki ambaye Marioo anamwamini sana kiasi kwamba hata akirekodi wimbo kwa mtayarishaji mwingine, basi atamsikilizisha kwanza ili aone kama kila kitu kipo sawa.
Hiyo ni kwa sababu Abbah ndiye alimtoa Marioo kimuziki kupitia wimbo, Dar Kugumu (2018), na pia amehusika katika nyimbo zake nyingi za mwanzo zilizompatia umaarufu.
2. Marioo ndiye aliyeandika wimbo wa Abigail Chams, Nani? (2023) ambao kashirikishwa pia. Ila baada ya hapo waliingia katika mzozo baada ya Marioo kufuta vesi ya Abigail katika wimbo wake, Love Song (2023).
3. Alikiba kutokea Kings Music ndiye alikuja kuchukua nafasi ya Abigail katika wimbo huo, kitendo kilicholeta maneno mengi hadi kumhusisha Paula.
4. Mpenzi wa Marioo, Paula ametokea katika video nyingi za nyimbo za mwanamuziki huyo ila iliyotazamwa zaidi katika mtandao wa YouTube ni ile ya mwisho kuachiwa, nayo ni Tete (2025).
Video ya wimbo huo ndani ya miezi sita imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 32, ikipanda hadi nafasi ya nne katika orodha ya nyimbo zake zilizofanya vizuri katika mtandao huo.
5. Kabla ya Tete (2025), Paula alishaonekana katika video nyingi za Marioo kama Lonely (2023), Tomorrow (2023), Sing (2023), Hakuna Matata (2024), Unachekesha (2024) na My Daughter (2024).
6. Hivyo Marioo ndiye mwanamuziki aliyetoa video nyingi na Paula hadi sasa lakini Rayvanny anasalia kuwa staa wa kwanza Bongo kufanya kazi na mrembo huyo aliyetokea katika video yake, Wanaweweseka (2021).
7. Kolabo yao ya kwanza, Tonge Nyama (2025) ilikuja miaka minane tangu Marioo alipomwandikia Nandy wimbo, Wasikudanganye (2017) ambao tayari alikuwa ameshaurekodi kwa Bonga.
Chanzo; Mwananchi Scoop