Moscow, Februari 5 — Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amezindua rasmi Mwaka wa Umoja wa Mataifa ya Watu wa Urusi, mpango wa kitaifa utakaotekelezwa katika mwaka 2026. Tangazo hilo lilitolewa katika Kituo cha Kitaifa cha “Russia” wakati wa marathon ya “Russia — Family of Families” iliyoandaliwa na Znanie Society.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Putin alisisitiza kuwa licha ya tofauti za kikabila, kitamaduni na kilugha zilizopo nchini humo, wananchi wa Urusi wameunganishwa na maadili ya pamoja. Alieleza kuwa katika nyakati zote, Warusi wamekuwa wakiunganishwa na dhamira ya kulinda ardhi yao ya pamoja, familia zao, pamoja na kuhifadhi utamaduni na mila zao.
Sherehe ya uzinduzi pia ilihudhuriwa na Naibu Waziri Mkuu wa Shirikisho la Urusi, Tatyana Golikova, ambaye alifungua rasmi marathon ya “Russia — Family of Families.” Katika hotuba yake, alisisitiza kuwa kila taifa ndani ya Urusi lina upekee wake, na kwamba maelewano pamoja na umoja vimekuwa sifa kuu ya mwingiliano wa watu wa nchi hiyo.

Katika jukwaa kuu la marathon hiyo, viongozi wa serikali, wanasayansi, wabunifu wa sanaa na michezo, pamoja na Mashujaa wa Urusi walizungumza na vijana kuhusu umuhimu wa umoja wa mataifa ya Urusi, urithi wa kitamaduni, nafasi ya lugha ya Kirusi, pamoja na ushindi na mapambano ya taifa hilo katika kutetea ukweli.
Zaidi ya watu 5,600 waliowakilisha mataifa 194 ya nchi hiyo walishiriki katika hafla hiyo. Kupitia mkutano wa mtandao (teleconference), wawakilishi kutoka mikoa yote 89 ya Urusi walijiunga na sherehe ya uzinduzi kwa njia ya mtandao, jambo lililoonesha ushiriki mpana wa kitaifa.

Kabla ya uzinduzi rasmi, jumla ya watu 39,065 walishiriki katika kampeni ya #WEARERUSSIA, wakishirikisha mila za familia zao na kuchapisha picha pamoja na video kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia alama ya reli (hashtag) #WEARERUSSIA.
Mwaka wa Umoja wa Mataifa ya Watu wa Urusi unatarajiwa kuwa kampeni kubwa ya kitaifa yenye lengo la kuimarisha mshikamano wa kiraia na kuendeleza utambulisho wa pamoja wa taifa.