Mwanamuziki wa Nigeria, Tiwa Savage ametaja orodha ya wasanii watatu anaowakubali likiwemo jina la msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz.
Tiwa yupo Marekani kwenye ziara ya kutangaza albamu yake mpya iitwayo This is Personal itakayoachiwa hivi karibuni.
Akizungumza kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Hot97 nchini Marekani, mkali huyo wa Afrobeat alitakiwa kuwataja wasanii watatu Afrika anaowakubali na wanaofanya vizuri.
Tiwa alieleza kuwa Diamond ni msanii mwenye kipaji kikubwa na anaiweka Tanzania kwenye ramani ya muziki kimataifa.
"Nampenda Diamond kutoka Tanzania ni balozi wa muziki wa Bongo, ni msanii wa kushangaza, ana kipaji kikubwa mimi na wenzangu tunajivunia kuwa mabalozi wa muziki wa Afrika," alisema mwanadada huyo.
Hii sio mara ya kwanza kwa Diamond kutajwa na wasanii wakubwa kuwa nyota anayefanya vizuri kimataifa na miongoni mwao ni Mmarekani Ciara aliyeshirikisha naye kwenye ngoma ya Low iliyotoka hivi karibuni.
Ikumbukwe Diamond na Tiwa waliwahi kufanya kazi pamoja mwaka 2017 kupitia wimbo wa Fire uliofanya vizuri na kuwa zaidi ya watazamaji milioni 12 katika mtandao wa Youtube.
Chanzo; Mwananchi Scoop