Mwanamitindo na mwanzilishi wa kampuni ya Rhode, Hailey Bieber, 29, amefunguka kuhusu maisha yake ya ndoa akisema anatamani kuongeza watoto zaidi katika familia yao lakini hana haraka.
Hailey ambaye yupo katika ndoa na Justin Bieber, 31, tangu mwaka 2018, pia alieleza mapenzi yake katika muziki wa mumewe akitaja albamu mbili anazozikubali zaidi kutoka kwake.
Akizungumza na Podcast ya Therapuss, Hailey alisema mtoto wao wa pekee, Jack Blues Bieber mwenye umri wa miezi 16, tayari ameanza kuonyesha dalili za kurithi kipaji cha muziki kutoka kwa baba yake.
Katika Podcast hiyo inayoendeshwa na Jake Shane, mrembo huyo alieleza namna mtoto wao alivyoanza kuimba wimbo maarufu wa Justin Bieber, Baby (2010).
“Ndiyo anafanya hivyo. Amekuwa akisema, ‘Baby, oh baby, oh baby oh.’ Na mimi nikawa kama, ‘wow, hiyo ni nzuri sana,’” alisema Hailey.
Alieleza kuwa tayari Jack anaongea maneno kadhaa na anaonesha wepesi wa kujifunza, mathalani kila mara anatamka neno ‘basketball’ kwa sababu ni moja ya michezo anayoipenda baba yake.
“Anaongea sana kwa umri wake. Anasema ‘basketball’ muda wote... Pia alijua kusema ‘sorry’ kwa lugha ya alama kabla hata hajaanza kulitamka neno hilo kwa sauti,” ameeleza.
Kuhusu uzazi, Hailey alisema siku zote alijua kuwa anataka kuwa mama na amefurahia kila hatua ya safari hiyo. Alipoulizwa kama yeye na Bieber wamepanga kupata watoto zaidi, alijibu ‘ndiyo’ bila kusita.
Chanzo; Mwananchi