Ushindani wa Tyla, 24, katika tuzo za Grammy, kwa mara nyingine umegeuka mwiba kwa mashabiki wa tasnia ya muziki huko Nigeria hasa wale wa Davido, 33, ambao wanalalamika wakidai alistahili ushindi.
Hata hivyo, Tyla kutokea Afrika Kusini, hana namna zaidi ya kuendelea kufanya kile anachofanya mara zote, na kwa muktadha huo, mashabiki wa Davido na wa washindani wengine wajiandae kulia zaidi!.
Katika tuzo za 68 za Grammy 2026 zilizotolewa wikiendi iliyopita huko Los Angeles, Marekani, Tyla alishinda kipengele cha ‘Best African Music Performance’, ambacho ni maalumu kwa muziki wa Afrika.
Ushindi huo wa Tyla umekuja kupitia wimbo wake, Push 2 Start (2024), ambao umewazidi kete washindani wake; Burna Boy (Love), Davido (With You), Eddy Kenzo (Hope & Love) na Ayra Starr (Gimme Dat).
Hii inakuwa mara ya pili kwa Tyla kushinda kipengele hicho kilichotambulishwa na waandaaji wa tuzo hizo, Recording Academy kwa mara ya kwanza hapo Juni 2023, na kuanza kutumika msimu wa 2024.
Lakini kwa nini mashabiki wengi wa Davido wanalalamikia ushindi wa sasa wa Tyla? Ingawa zinatajwa hoja nyingi ambazo baadhi zinakosa uthibitisho kabisa, ila kuna moja naweza kuizungumzia.
Katika kiwanda cha muziki Nigeria kuna kile wanachoita ‘Big Three’ wakimaanisha wasanii wakubwa watatu ambao ndio hasa wenye ushawishi mkubwa na ndio wanaoibeba tasnia hiyo kwa wakati huo.
Utatu huo unaundwa na Burna Boy, Wizkid na Davido mwenyewe, lakini baadhi ya wasanii wengine akiwamo Tiwa Savage, wamekuwa wakipinga hilo wakisema muziki wa Nigeria ni zaidi ya watatu hao.
Sasa katika hawa watatu, ni Davido peke yake ndiye hajashinda tuzo ya Grammy, na hii mara zote imetumika na mashabiki wa washindani wake kama fimbo ya kumchapia wakidai hastahili kuwamo katika ‘Big Three’.
Na hilo hasa ndio limekuwa likiwapa hasira mashabiki wa Davido, wao wanaona anastahili kushinda Grammy bila kujali kama ana kazi nzuri, bali wanachohitaji ni kutimiza matakwa yao ya kiushindani katika soko la Nigeria.
Chanzo; Mwananchi Scoop