Mahakama ya Los Angeles imeidhinisha kuendelea kwa kesi nzito ya madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya gwiji wa muziki Sean “Diddy” Combs. Hatua hiyo imekuja baada ya jaji kukataa maombi ya kuitupilia mbali kesi hiyo.
Kesi hiyo ilifunguliwa na mtayarishaji wa muziki Jonathan Hay, anamshitaki Diddy kwa madai ya kumpiga, kumfungia na kumnyanyasa kingono wakati wa walipokuwa studio wakirekodi muziki mwaka 2020. Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, Hay anadai kuwa alifunikwa uso, kupigwa kisha kulazimishwa kufanya kitendo cha kingono bila ridhaa yake.
Hay pia anadai kuwa kabla ya tukio hilo, Diddy alikuwa akimpatia dawa za kulevya ikiwemo ketamine wakati wanapokuwa studio. Aidha, madai hayo yaliyowasilishwa mahakamani yanahusisha pia mirathi ya marehemu rapa The Notorious B.I.G. zinazosimamiwa na mwanawe Christopher “CJ” Wallace.
Anadai kuwa baada ya tukio hilo la unyanyasaji kukamilika, Diddy alifanya kitendo cha ajabu na cha kudhalilisha kwa kumtupia usoni fulana iliyokuwa ikimilikiwa na Biggie Smalls, huku akisema, “Pumzika kwa amani, BIG.”
Akizungumza katika mahojiano na gazeti la The Post, Hay alisema uamuzi wa mahakama ni “wiki kubwa” kwake, ingawa ni sehemu ya kipindi kigumu na kibaya sana katika maisha yake. Alieleza kuwa awali alikuwa na furaha kubwa kushiriki katika mradi uliomhusisha marehemu The Notorious B.I.G., aliyefariki kwa kupigwa risasi katika shambulio la gari mwaka 1997 huko Los Angeles.
“Nilikuwa shabiki mkubwa wa Biggie, ndiyo maana tulianza mradi huu. Ilikuwa heshima kufanya kazi na mirathi yake,” alisema Hay kabla ya kuongeza kwa huzuni, “Lakini Sean Combs alikuja na kufanya kila kitu kuwa giza.”
Chanzo; Mwananchi Scoop