Ndugu wawili Siyabonga Gezani na Malusi Dave Ndimande wamerejeshwa Afrika Kusini kwa ajili ya kukabiliana na mashtaka yanayowakabili dhidi ya kifo cha rapa AKA na mpishi Tibz.
Ndugu hao waliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Shaka, Durban, Jumanne Novemba 11, 2025 ambapo walikabidhiwa kwa polisi wa SAPS.
Awali, ndugu hao walikuwa wakijificha Eswatini baada ya kutuhumiwa katika mauaji hayo mapema mwaka 2024. Walipokamatwa walipinga kurejeshwa Mzansi kwa sababu za usalama, lakini rufaa zao zilikataliwa na kuamuliwa na mahakama kurejea Mzansi.
Polisi walisema ndugu hao wanakabiliwa na mashtaka 24 katika kesi tatu tofauti, mauaji ya afisa wa taxi Manzimtoti 2022 (mashtaka 5), mauaji ya AKA na Tibz (mashtaka 11), na mauaji ya afisa mwingine wa taxi huku wakijaribu kumuua mkewe (mashtaka 8).
Ndugu hao waliungana na watuhumiwa wengine Mahakama ya Manispaa ya Durban siku ya Jumanne, Novemba 11, 2025 ambao ni Lindokuhle Mkhwanazi, Lindani Ndimande, Siyanda Myeza, Mziwethemba Gwabeni na Lindokuhle Mkhwanazi, ambao tayari walikamatwa Mzansi huku kesi hiyo ikianza kusikilizwa tena Juni 26,2026 baada ya dhamana yao kukataliwa.
Kiernan “AKA” Forbes (35), alifariki dunia Februari 10, 2023, baada ya kupigwa risasi mara kadhaa akiwa nje ya mgahawa jijini Durban, KZN.
Chanzo; Mwananchi Scoop