Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya historia ya www.countryliving.com, wakati wa karne ya tano kulikuwa na kiongozi aliyeitwa Mfalme Claudius II ambaye aliamini askari anapooa hawi mkakamavu na pia muda mwingi anawaza kuhusu familia yake, zaidi ya kitu kingine chochote.
Hivyo, alipiga marufuku ndoa kwa askari. Kitendo hicho hakikuwafurahisha watu wengi, akiwamo Padri Valentino.
Kiongozi huyo wa kidini aliendelea kufungisha ndoa kwa siri. Mfalme Claudius alipopata habari hizo aliamuru Padri Valentino akamatwe na kuuawa.
Mtakatifu Valentino aliuawa Februari 14, ndiyo maana ikatangazwa rasmi kuadhimishwa kwa ajili ya kumkumbuka kama baba wa upendo na mtetezi wa wanandoa. Historia inaonyesha kuwa aliyetangaza kuadhimisha siku hiyo ni Papa Gelasius.
Pia, ipo simulizi nyingine inayosema akiwa gerezani kwa amri ya Mfalme Claudius, Padri Valentino aliandika barua iliyokuwa na salamu kwa binti aliyekwenda kumsalimia gerezani mara kwa mara kabla ya hukumu ya kifo chake. Mwisho wa barua alihitimisha kwa kusema ‘Kutoka kwa Valentino wako’. Tangu hapo, Valentino anakumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na sikukuu yake huadhimishwa ulimwenguni kote.
Kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa Katoliki, baadaye, Padri Valentino alikuja kutangazwa kuwa Mtakatifu.
Namna watu wanavyoisherehekea katika karne ya sasa
Tofauti na zamani ambapo maadhimisho yalijikita zaidi kwenye kubadilishana kadi na maua, sasa watu huadhimisha kwa njia mbalimbali zinazoendana na mtindo wa maisha ya kisasa. Wengi hutumia siku hiyo kuwapelekea wapendwa wao zawadi kama maua, chokoleti, manukato na vitu vingine vya thamani kama ishara ya upendo na kuthaminiana.
Chanzo; Mwananchi Scoop