Mtangazaji wa Clouds Media Group na mdau mkubwa wa maendeleo ya sanaa nchini, Miss Loloh, ametoa elimu kwa wasanii wapya kuhusu umuhimu wa meneja katika safari yao ya muziki.
Loloh ameeleza kuwa msanii mwenye meneja ana nafasi kubwa ya kufanikisha ndoto zake, kwani meneja husaidia kupanga, kusimamia, na kuongoza shughuli za msanii kwa weledi, hivyo kumpunguzia mzigo wa majukumu na kumuongoza katika njia sahihi ya mafanikio.
"Kama una ndoto ya kufika mbali kupitia kipaji chako, hakikisha una MANAGER.
Huyu anaweza kuwa kaka yako, dada yako, mshikaji, ndugu, au mtu yeyote mwenye uelewa wa muziki. Manager atakusaidia kujiandaa vizuri ukipata nafasi kwenye media. maana kazi yako kama msanii ni kumaliza hasira yako studio, mengine atakuwa anakusaidia"--Ameandika Loloh.
Aidha, amewashauri wasanii chipukizi kujifunza namna ya kujieleza vizuri wanapokuwa mbele ya vyombo vya habari, pamoja na kuwa na mawasiliano mazuri na watu wanaowazunguka, jambo ambalo ni la msingi katika kujenga taswira chanya ya msanii na kukuza mahusiano ya kikazi.
"Kumbuka, Good music ni muhimu. Lakini jinsi unavyoweza kujielezea kutavutia watu wengi kukusikiliza na ukweli ni kwamba Msanii anayejua kuongea vizuri, ana nafasi kubwa ya kupenya kwenye game na kushawishi watu kufatilia kazi zake. Kuongea vizuri ni silaha ya msanii mwenye ndoto ya kuwa mkubwa!
Jifunze, jiandae, na usiogope kuomba msaada!" Ameeleza Loloh
Chanzo: Clouds Media