Nabii Richard Magenge, aliyekuwa msimamizi wa ndoa ya Emmanuel Mathias, maarufu MC Pilipili, amesema ameondokewa na kijana aliyekuwa na heshima, upendo na uaminifu mkubwa katika kazi na mahusiano ya kila siku.
Akizungumza jana, Magenge amesema alimfahamu kwa ukaribu kupitia kazi za sanaa na shughuli mbalimbali za kijamii, akimtaja marehemu kama msanii mwenye maono makubwa na mwenye moyo wa kusaidia watu. Alieleza kuwa MC Pilipili alikuwa amerejea jijini Dodoma kuendeleza kazi zake za sanaa pamoja na mikakati mingine aliyokuwa ameipanga.
Hata hivyo, Magenge amesema siku ambayo familia ilikuwa imepanga kufanya kikao maalumu, ndiyo siku ambayo msanii huyo alipoteza maisha, Novemba 16. Alisema tukio hilo limeiacha familia na watu wa karibu katika majonzi makubwa, kwani walikuwa wakitarajia kukutana kwa mazungumzo muhimu ya kifamilia.
Chanzo; Mwananchi