Msanii wa Bongo Fleva, Zuhura Othman Soud 'Zuchu', amesema hana mpango wa kuondoka kwenye lebo ya WCB Wasafi, kwani yuko kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanzilishi wa lebo hiyo, Diamond Platnumz.
Zuchu alisaini rasmi mkataba na WCB Aprili 2020, tangu hapo amekuwa miongoni mwa wasanii wa kike wanaofanya vizuri hapa nchini kwa sasa.
Kwa mujibu wa Daily Nation ambayo imefanya mahojiano na mwanadada huyo ambaye ni mke halali wa Diamond imeandika: “Nawatakia kila la heri wote waliotoka. Naelewa kuwa kuna wakati katika maisha mtu hutamani kukua. Lakini kwangu mimi, sioni sababu yoyote ya kuondoka WCB. Mwisho wa siku, nina mahusiano na bosi wa lebo (tuko kwenye uhusiano wa kimapenzi)."
Mwaka 2022 Diamond Platnumz aliweka wazi kuwa endapo Zuchu atahitaji kuvunja mkataba wake kabla ya muda, itamlazimu kulipa Sh10 bilioni, kiasi ambacho kinaonyesha ukubwa wa thamani yake kwenye lebo hiyo.
Kiasi hicho kinaonyesha ukubwa wa uwekezaji ambao WCB imefanya katika kukuza kazi ya Zuchu kuanzia ubunifu wa chapa (branding), matangazo, masoko, uzalishaji wa muziki, hadi ushirikiano na wasanii wakubwa.
Chanzo: Mwananchi Scoop