Waswahili husema “mkataa kwao mtumwa”. Hivyo basi mwanamuziki wa Bongo Fleva Kusah ameukataa utumwa baada kwenda kuzindua EP yake ‘Bumbuli Boy’ nyumbani kwao Bumbuli mkoani Tanga.
Akizungumza na Mwananchi , Kusah amesema sababu iliyopelekea kufanya hivyo ni kubadilisha mtazamo wa vijana waliokata tamaa.
“Mimi nimeamua kuifanya hii kitu local kabisa na iwe kijijini kwetu ili kuwapata watu wote, hata ambao nilikuwa nikiwamisi. Nimetokea, nimesoma Bumbuli najua changamoto za vijana wengi.
“Najua vitu vinavyowakumba watu wengi huku, sio tu nimekuja kufanya Ep ya Bumbuli Boy. Nimekuja kuongea na vijana kubadilisha mtazamo wao kwa sababu sisi ni kioo cha jamii muda mwingine tunavyoongea inakuwa rahisi wao kuwafikia,”amesema
Kusah amesema kuna utofauti mkubwa kati ya vijana wa kipindi chake na vijana wa sasa. Hivyo Bumbuli Boy ni kwaajili ya kuwapa hamasa na kurudi kwenye mstari. “Zamani wakati mimi nasoma tulikuwa tukitoka shuleni tunaenda mpirani au umechukua boda yako kwa hiyo tulikuwa bize sana. Lakini sasa hivi wanakunywa pombe, wala hawana watu wa kuwahamasisha,” amesema Kusah.
Chanzo; Mwananchi Scoop