Msanii wa Hip Hop kutoka Marekani, 50 Cent, alianza kuwa baba kabla hajapata mafanikio makubwa katika muziki lakini uhusiano kati yake na mwanaye mkubwa, Marquise, 29, umekuwa na misukosuko mingi.
Kwa muda mrefu wawili hao wamekuwa hawapatani na hata kuvunjiana heshima, huku migogoro yao mingi kuhusu malezi na fedha ikijadiliwa kwa uwazi mkubwa kupitia mitandao ya kijamii.
Mkali huyo wa kibao cha In Da Club (2003), alijaliwa mtoto huyo mnamo Oktoba 1996 katika uhusiano na aliyekuwa mpenzi wake, Shaniqua Tompkins ambaye waliachana kwa drama nyingi.
Wazazi hao walikuwa pamoja miaka ya 1990, uhusiano ambao kwa muda mrefu ulibeba tabia ya kuvunjika na kurudiana, kisha kuja kuachana kabisa ila waliendelea kuvutana mahakamani kuhusu malezi.
Kwa ujumla, 50 Cent ni baba wa watoto wawili, mwingine ni Sire Jackson (2012) aliyezaa na Daphne Joy kabla ya kuachana. Na kwa leo, tutaangazia mgogoro kati yake na mtoto wake mkubwa, Marquise.
Baada ya kuachana, 50 Cent na mzazi mwenzie, Shaniqua waliingia kwenye mvutano mkali na wa muda mrefu wa kisheria kuhusu malezi ya Marquise, mgogoro ambao haukupata muafaka rasmi hadi Oktoba 2008.
Wakati wa mzozo huo, 50 Cent alikiambia kituo cha MTV kuwa uhusiano wake na mwanaye umebadilika kwa kiasi kikubwa na hiyo ni kwa sababu yeye na mama mtoto hawakuwa tena marafiki.
Chanzo; Mwananchi Scoop