Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo , ametembelea Ofisi za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) jana Jijini Dodoma, kwa lengo la kujiunga na elimu ya sekondari kwa njia mbadala.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka taasisi hiyo, Baba Levo alipatiwa maelezo mahsusi pamoja na taratibu za kujiunga na masomo ya sekondari kupitia TEWW, na tayari amepewa 'control number' (namba ya malipo serikalini) kwa ajili ya kulipia ada ili aanze masomo yake mara moja.
TEWW imeeleza kwamba hatua hiyo inaakisi dhamira yake (Baba Levo) ya kuthamini elimu kama nguzo ya maendeleo binafsi na ya jamii.
Baba Levo aliambatana na Asha Feruzi , Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha vyuo na vyuo vikuu, ambaye kabla ya kuingia bungeni alikuwa Mhadhiri Msaidizi wa TEWW.
TEWW ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 12 ya mwaka 1975, pamoja na majukumu mengine, ikiwa na jukumu la kutoa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi kwa rika zote, ili kuchochea maendeleo endelevu ya Watanzania.
Chanzo; Nipashe