Nyota wa Afrobeat kutoka Nigeria, Burna Boy amejikuta katika mgogoro wa kisheria kufuatia na umiliki wa katalogi ya nyimbo zake za mwanzo ambazo zilimpatia umaarufu.
Mgogoro huo ni baina ya lebo yake ya zamani ijulikanayo kama ‘Aristokrat Records’ na menejimenti yake ya sasa ya Spaceship Music, huku kampuni ya uwekezaji ya 960 Music Group nayo ikipeleka kesi yao mahakamani.
Taarifa zinaeleza kuwa chanzo cha mvutano huo ni makubaliano yaliyofanyika katikati ya mwaka 2024, ambapo Aristokrat Records ilidaiwa kuuza haki miliki (IP) pamoja na master recordings za nyimbo za zamani za Burna Boy, ikiwemo Like to Party na Tonight kwenda Spaceship Music, lebo inayomilikiwa na msanii huyo na kusimamiwa na mama yake, Bose Ogulu.
Hata hivyo, 960 Music Group, ambayo inamiliki asilimia 40 ya hisa ndani ya Aristokrat Records, imepinga mauzo hayo ikidai yalifanyika bila idhini yao kama wanahisa wakubwa wa kampuni.
Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa kampuni hiyo, amesema “Huwezi kuuza asilimia 100 ya mali wakati unamiliki asilimia 60 tu. Tunaamini kulikuwa na juhudi za kuhamisha haki hizi kwa siri, ndiyo maana tumekimbilia mahakamani ili mali hizo zirudishwe,” alinukuliwa akisema mtendaji huyo.
Kutokana na hali hiyo, 960 Music Group imefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Shirikisho zilizopo Lagos na Port Harcourt ikiomba mauzo hayo yatangazwe kuwa batili, ikisisitiza kuwa uamuzi huo ulifanyika bila wao kufahamishwa, bila ridhaa yao na bila kupitishwa na bodi ya wakurugenzi.
Chanzo; Mwananchi Scoop