Nguli wa filamu kutoka Hong Kong, Jackie Chan, amefichua kuwa amerekodi wimbo ambao utaachiwa baada ya kifo chake. Wimbo ambao utapigwa siku mwili wake utakapoagwa na watu mbalimbali.
Chan mwenye umri wa miaka 71 alitoa taarifa hiyo wakati wa uzinduzi wa filamu jijini Beijing, akisema kwa miaka ya hivi karibuni amekuwa akijitafakari kuhusu maisha, uzee na kifo. “Najiuliza mara nyingi nitakuwaje mwisho wangu. Labda nifanye tukio hatari, nife na nibaki kuwa hadithi,”amesema
Chan pia alisema kupoteza ndugu na marafiki wa karibu wengi katika miaka ya karibuni kumemfanya azidi kufikiria sana masuala ya maisha na mwisho wa binadamu. “Watu wote watazeeka mwisho wa siku, na ni jambo la kufurahisha kuzeeka taratibu. Sisi wazee tuna bahati sana,” amesema Chan
Aidha kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Singapore, 8days, Chan amekuwa akiomboleza vifo vya marafiki wake kadhaa wa karibu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Miongoni mwa watu waliopoteza maisha ambao amekuwa akiwakumbuka zaidi ni nyota wa sanaa za mapigano Cheng Pei Pei na Corey Yuen, mtunzi wa nyimbo kutoka Taiwan Liu Chia Chang, mwigizaji wa Hong Kong Li Lili, pamoja na mchambuzi wa masuala ya chakula Chua Lam.
Ripoti za hivi karibuni pia zinaonyesha kuwa Chan amekuwa akijitahidi kurejesha uhusiano na binti yake Etta Ng Chok Lam, ambaye alizaliwa nje ya ndoa ili kuhakikisha haondoki duniani akiwa na kinyongo na mtu yoyote. Aidha hatua hiyo imewashangaza mashabiki huku wengi wakibaki na maswali wakidhani huwenda mwigizaji huyo kuna ugonjwa unamsumbua.
Chanzo; Mwananchi Scoop