Rais wa Marekani, Donald Trump ameishutumu hafla ya ugawaji wa tuzo za Grammy, iliyofanyika Jumapili, Februari 1, 2026 na kutishia kumshtaki mchekeshaji Trevor Noah, ambaye alikuwa mshereheshaji wa tuzo hizo. Kutokana na mzaha aliofanya kuhusu Trump na Bill Clinton kudaiwa kutembelea kisiwa cha Jeffrey Epstein
Katika ujumbe uliochapishwa katika mtandao wa Truth Social, Trump aliandika kuwa tuzo hizo ni mbaya zaidi.
“Tuzo za Grammy ndiyo mbaya zaidi, ambazo haziwezi hata kutazamwa. CBS ina bahati ya kutokuwa na takataka kama hii tena,” alisema hivyo akirejelea Disney kuchukua haki za utangazaji wa sherehe hizo kuanzia mwaka ujao.
"Noah alisema uwongo kunihusu, kwamba Donald Trump na Bill Clinton walitumia muda wao katika Kisiwa cha Epstein. Si kweli! Siwezi kumzungumzia Bill, lakini sijawahi kwenda kisiwa cha Epstein, wala mahali popote karibu na hapo. Hadi taarifa ya uwongo na ya kuniharibia sifa usiku wa leo, sijawahi kushtumiwa kuwa huko, siyo hata na vyombo vya habari bandia,” amesema Trump.
Hatahivyo Trump amemuonya Noah, akisema ni bora aeleze ukweli wake kwa usahihi, vinginevyo atamfungulia mashtaka na kumtaka amlipe pesa nyingi.
"Inaonekana kama nitawatuma wanasheria wangu kumshtaki mshereheshaji huyu maskini, mwenye kusikitisha, asiye na kipaji, na mlaghai. Nitamshtaki mchekeshaji huyo anilipe pesa nyingi. Jiandae Noah, tutapambana!” alisema Trump.
Chanzo; Mwananchi Scoop