Tarehe 29 Desemba 2025, bondia maarufu Anthony Joshua, alijikuta katika ajali mbaya ya barabara nchini Nigeria katika barabara ya Lagos–Ibadan Expressway katika eneo la Makun, Mkoa wa Ogun. Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wawili waliokuwa na uhusiano mkubwa na Joshua, huku yeye mwenyewe akipata majeraha madogo na kupelekwa hospitalini.
Polisi wamebainisha kwamba watu wawili waliopoteza maisha walikuwa marafiki wa karibu na wanachama wa timu yake ya mazoezi ambao wametambulika kama;
Sina Ghami – Alikuwa mkufunzi wa nguvu na utayari (strength & conditioning coach) wa Joshua
Kevin “Latif” Ayodele – Alikuwa mkufunzi wa kibinafsi (personal trainer) wa Joshua na mmoja wa watu waliokuwa karibu sana naye.
Wote wawili walifariki ghafla pale gari walilokuwa wakisafiria lilipogongana na lori lililokuwa limeegeshwa pembeni ya barabara.
Sina Ghami na Latif Ayodele walikuwa si tu wafanyakazi wa timu ya Joshua bali marafiki wa karibu wa kibinafsi waliokuwa sehemu ya maandalizi yake ya mazoezi na safari zake za kazi. Walikuwa na jukumu muhimu katika utayarishaji wa Joshua kabla na baada ya mechi zake, jambo lililifanya vifo vyao kuwa pigo kubwa kwa mwanamasumbwi huyo.
Uchunguzi wa awali kutoka kwa Federal Road Safety Corps (FRSC) ya Nigeria unaonyesha kwamba gari lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo kasi kupita kiwango kilichoruhusiwa huku likijaribu kupita gari jingine hali iliyosababisha kupoteza udhibiti na kugonga lori lililokuwa limeegeshwa kwa upande wa barabara.
Anthony Joshua ambaye pia ana asili ya Nigeria mara nyingi amekuwa akirudi nchini Nigeria kufanya shughuli za kibinafsi na mazoezi.
Ajali hii ilitokea karibu siku chache tu baada ya Joshua kushinda mechi yake dhidi ya Jake Paul huko Miami na ilileta mshtuko kwa mashabiki duniani kote.
Serikali ya Nigeria na vyombo vya usalama wametoa pole kwa familia za waliofariki na kuahidi uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha ajali.
Chanzo; Eatv