Winga wa zamani wa Manchester United, Antony, ametoa malalamiko kuhusu namna alivyotendewa vibaya wakati akiwa sehemu ya wachezaji waliotengwa ndani ya kikosi hicho chini ya kocha Ruben Amorim, kabla ya msimu huu kuondoka rasmi na kutua Real Betis.
Antony, ambaye alisajiliwa na Man United Agosti 30, 2022, kwa dau kubwa la pauni milioni 86 akitokea Ajax, aliishia kuwa moja ya usajili mbovu baada ya klabu hiyo kupata hasara ya karibu pauni milioni 60 katika mauzo yake dakika za lala salama ya dirisha la usajili lililopita.
Awali maisha yake ndani ya Man United yalikuwa mazuri akifanikiwa kusaidia kushinda mataji mawili, Carabao mwaka 2023 na Kombe la FA 2024. Baada ya hapo, mambo yakageuka.
Nyota huyo raia wa Brazil, ameeleza kuwa aliishi maisha magumu akiwa ameachwa nje ya kikosi cha kwanza, ambapo alitumia zaidi ya siku 40 akiishi katika hoteli ya uwanja wa ndege jijini Manchester, akilipa pauni 175 kwa usiku, huku akifanya mazoezi kivyake.
Akizungumza na El Desmarque, Antony amesema: “Ilikuwa miezi migumu sana nchini England, zaidi ya siku 40 hotelini, kufanya mazoezi peke yangu… Nahisi nilidharauliwa, lakini sitaki kuanzisha malumbano. Hayo ni maisha. Nashukuru kwa klabu, kulikuwa na nyakati mbaya na pia nzuri, tulipata mataji mawili.”
Antony ameweka wazi kuwa familia yake ilitangulia kuhamia Mji wa Seville siku chache kabla ya dili la kurejea Betis kukamilika, tayari akiwa ameshapangisha nyumba.
Chanzo: Mwanaspoti