Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetangaza kuchukua tahadhari zote za kiusalama kuelekea mechi ya Ngao ya Jamii kati ya klabu ya Yanga SC na Simba SC itakayochezwa Jumanne, 16 Septemba 2025 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, usalama katika eneo lote la uwanja, barabara za kuingia na kutoka, ndani na nje ya uwanja umeimarishwa kwa kiwango cha juu. Ukaguzi wa kina utafanyika kabla ya kuingia uwanjani, na hairuhusiwi mtu yeyote kuingia na silaha ya aina yoyote isipokuwa vyombo vya dola vilivyoidhinishwa.
Jeshi la Polisi limewaomba wapenzi wa soka kufuata taratibu, kuacha kutumia lugha za matusi au kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani. Polisi imesisitiza haitasita kuchukua hatua za haraka kwa yeyote atakayebainika kufanya makosa hayo.
Jeshi la Polisi Dar es Salaam limewatakia mashabiki wote na timu zote mchezo mzuri.
Chanzo: Global Publishers