Mshambuliaji wa Chichester City, Billy Vigar ambaye amepata mafunzo ya kisoka katika Akademi ya Arsenal, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 21 kufuatia jeraha kubwa la ubongo alilolipata katika mchezo wa Ligi ya Isthmian uliochezwa Jumamosi iliyopita dhidi ya Wingate & Finchley, mechi ambayo ilisitishwa dakika ya 13 baada ya tukio hilo.
Kupitia taarifa rasmi, klabu ya Chichester imesema: “Baada ya kupata jeraha kubwa la ubongo Jumamosi iliyopita, Billy Vigar aliwekwa katika koma.
"Jumanne alifanyiwa upasuaji uliolenga kuongeza nafasi ya kupona. Ingawa jitihada hizo zilisaidia kwa kiasi, jeraha hilo lilikuwa kubwa mno na alifariki Alhamisi asubuhi.”
Chichester pia imesema: “Majibu ya mashabiki na wadau wa soka tangu taarifa ya awali yalionyesha ni kwa kiasi gani Billy alipendwa na kuheshimiwa ndani ya mchezo huu.
"Familia yake imesikitishwa sana na tukio hili lililotokea wakati akiwa anafanya kile alichokipenda zaidi ambacho ni kucheza mpira wa miguu.”
Billy Vigar alijiunga na Akademi ya Arsenal Desemba 2017 akiwa na umri wa miaka 14 na alisaini mkataba hadi Julai 2022.
Akiwa mchezaji wa Arsenal, alicheza kwa mkopo Derby County (akichezea timu ya vijana chini ya miaka 21) na Eastbourne Borough, kabla ya kujiunga na Hastings United kwa uhamisho wa bure Julai 2024. Kabla ya kuanza msimu huu, alijiunga na Chichester City.
Chanzo: Mwanaspoti