Alex Honnold ameibua shangwe kubwa kutoka kwa umati wa watu waliokusanyika chini ya jengo la Taipei 101 baada ya kufanikiwa kupanda hadi juu ya mnara wa jengo hilo lenye urefu wa mita 508, sawa na ghorofa 101 juu ya ardhi.
Tukio hilo lilichukua takribani dakika 90 tangu alipoanza safari yake ya kupanda, huku maelfu ya watu wakifuatilia moja kwa moja mitaani na kupitia matangazo ya mubashara, limetokea leo Jumapili.
Akiwa amevaa shati jekundu la mikono mifupi, Honnold alipofika juu kabisa alipunga mikono yake juu ya kichwa kwa furaha, ishara iliyozidisha nderemo, makofi na kelele za shangwe kutoka kwa watazamaji.
Tukio hilo lilifanyika jijini Taipei, mji mkuu wa Taiwan, na kuvuta hisia za vyombo vya habari vya kimataifa kutokana na hatari na upekee wake.
Honnold, mpandaji maarufu wa miamba kutoka Marekani anayejulikana kwa kupanda bila kutumia kamba katika mazingira ya asili, safari hii pia hakutumia kifaa chochote lakini tahadhari kubwa ilichukuliwa kwa ajili ya usalama.
Hatua hiyo ililenga kupunguza hatari zinazoweza kusababishwa na urefu mkubwa wa jengo, miundo ya chuma na kioo, pamoja na upepo mkali unaopatikana katika maeneo ya juu.
Licha ya tahadhari hizo, upandaji huo ulihitaji umakini mkubwa, nguvu za mwili na uthabiti wa akili.
Jengo la Taipei 101 lina ghorofa 101 juu ya ardhi na ghorofa tano chini ya ardhi, na kwa miaka mingi lilikuwa miongoni mwa majengo marefu zaidi duniani.
Kupanda jengo hilo kutoka chini hadi juu ni changamoto kubwa hata kwa wapandaji wenye uzoefu mkubwa, jambo lililofanya tukio la Honnold kuonekana la kipekee na la kihistoria.
Chanzo; Global Publishers