Staa wa Inter Miami, Lionel Messi, anajiandaa kurudi kwenye klabu yake ya utotoni, Newell’s Old Boys, ambapo mazungumzo yanaendelea kati ya mchezaji huyo na klabu hiyo maarufu ya Argentina.
Messi, mwenye umri wa miaka 38, alianza safari yake ya soka katika akademi ya Newell’s, akichezea timu za vijana kwa miaka saba kabla ya kujiunga na Barcelona akiwa na umri wa miaka 13. Amefunga mabao 234 akiwa na timu hizo za vijana, na hata kuna jukwaa la klabu limepewa jina lake!
Makamu wa rais wa Newell’s, Juan Manuel Medina, alisema:
“Tunafanya kazi kuhakikisha Leo anachezea Newell’s katika nusu ya kwanza ya mwaka 2027. Hili ni jambo kubwa si kwa Newell’s tu, bali kwa Jiji la Rosario na soka la Argentina kwa ujumla.”
Hata hivyo, Messi bado ana mkataba na Inter Miami hadi 2028, lakini kuna uwezekano wa kuhamia kwa mkopo wa muda mfupi ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuichezea klabu yake ya nyumbani.
Messi aliwahi kusema: “Ndoto yangu ni kuichezea Newell’s, lakini familia yangu ndiyo kipaumbele kwa sasa. Nataka wawe salama na wafurahie maisha.”
Tangu ajiunge na Inter Miami, Messi amecheza mechi 88, kufunga mabao 77 na kusaidia klabu hiyo kushinda MLS Cup, MLS Supporters’ Shield na Leagues Cup.
Chanzo; Mwanaspoti