Nyota wa timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo na bilionea Elon Musk walikuwa miongoni mwa wageni wa heshima katika hafla ya kifahari ya chakula cha jioni Ikulu ya White House, iliyoandaliwa na Rais wa Marekani Donald Trump kwa ajili ya kumkaribisha Mwana Mfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 40 na anayekipiga katika klabu ya Saudi Al Nassr, alifika muda mfupi kabla ya kuingia kwa Trump na Mohammed bin Salman.
Mkataba wa nyota huyo na Al Nassr unatarajiwa kumalizika majira ya kiangazi mwaka huu, jambo linalozua maswali kuhusu mustakabali wake wa soka.
Katika hotuba yake kabla ya dhifa hiyo, Trump alisema, "Unajua, mwanangu ni shabiki mkubwa wa Ronaldo."
Kiongozi huyo wa Marekani aliongeza kuwa mwanawe Barron Trump, mwenye umri wa miaka 19 na anayependa sana soka, alipata nafasi ya kukutana na gwiji huyo wa kandanda. "Nadhani sasa anamheshimu baba yake zaidi, kwa sababu tu nimemkutanisha na Ronaldo."
Ronaldo hakuwa mgeni pekee wa soka katika hafla hiyo. Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino, pia alikuwepo, akionekana kuendeleza uhusiano wake wa karibu na Ikulu ya White House kuelekea maandalizi ya Kombe la Dunia la 2026 ambalo Marekani itakuwa mwenyeji mwenza.
Chanzo; Dw