Mjadala mzito umeibuka mitandaoni nchini Tanzania kufuatia tukio la kunyimwa penati ya wazi kwa Timu ya Taifa katika mechi dhidi ya Morocco, tukio lililotokea dakika za mwisho za mchezo na kuzua hisia kali miongoni mwa mashabiki na wachambuzi wa soka.
Badala ya kubaki katika mjadala wa michezo pekee, Watanzania wengi wameupeleka mjadala huo katika uwanja mpana zaidi wa kijamii na kisiasa, wakitumia tukio hilo kama kielelezo cha hoja pana kuhusu mgongano kati ya haki na amani. Wapo wanaohoji ikiwa kunyamaza kwa jina la amani kunaweza kuhalalisha kunyimwa haki za msingi.
Katika mitazamo inayosambaa kwa kasi, baadhi ya wachangiaji wanasema tukio hilo linafundisha kuwa amani isiyojengwa juu ya haki ni kivuli kisicho na ulinzi, wakionya kuwa mtu au taifa linaweza kupoteza mambo muhimu endapo litajificha nyuma ya wito wa amani bila kudai haki yake kwa uwazi.
Mjadala huo umeendelea kuchochea fikra mpya miongoni mwa Watanzania, huku kauli inayojitokeza zaidi ikisisitiza kuwa haki ndiyo msingi wa amani ya kweli, na bila haki, amani hubaki kuwa neno tu lisilo na maana halisi.
Chanzo; Cnn