Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Dkt. Patrice Motsepe, amekanusha vikali taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari zikidai kuwa Tanzania, Kenya na Uganda zimepokwa uenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwaka 2027.
Akizungumza na waandishi wa habari hii leo Dar Es Salaam, Motsepe amesema “Katika siku za hivi karibuni nimeona taarifa kwenye mitandao ya kijamii na hata kwenye magazeti, ikiwemo The Guardian ya London, zikidai kuwa nimekuja kuwaambia Tanzania, Kenya na Uganda kwamba nitachukua AFCON kwa sababu nchi hizi hazitakuwa tayari. Hiyo si kweli kabisa,”
Motsepe amesisitiza kuwa CAF inaendelea kushirikiana na nchi hizo tatu katika maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027 na hakuna uamuzi wowote uliolenga kubadili uenyeji wa mashindano hayo. Kauli hiyo imekuja wakati wa mkutano wa CAF uliofanyika jijini Dar es Salaam, huku nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zikiendelea na maandalizi ya pamoja ya kuandaa AFCON2027.
Chanzo; Eatv