Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema Tanzania ipo tayari kuishangaza dunia kwa kuandika historia nyingine ya kuifunga Morocco katika mchezo wa hatua ya mtoano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 unaotarajiwa kuchezwa Jumapili, Januari 4, 2026.
Makonda ametoa kauli hiyo jana Januari 2, 2026, alipokutana na wachezaji na benchi la ufundi la timu ya Taifa, Taifa Stars, nchini Morocco, akiwa katika ziara ya kuwatia moyo kuelekea mchezo huo muhimu.
Amesema Stars ina kila sababu ya kuamini ushindi na kuwataka wachezaji kupambana kwa nidhamu na kujituma uwanjani ili kupata matokeo mazuri dhidi ya wenyeji.
“Tunakwenda kucheza mchezo mkubwa, lakini nina imani na kikosi hiki. Msisikilize kelele za mashabiki wa Morocco, waamini kuwa Watanzania wote wapo nyuma yenu na wanawaunga mkono,” amesema Makonda.
Stars itavaana na Morocco kesho kwenye mchezo wa hatua ya 16 Bora wa Kombe la Mataifa Afrika AFCON 2025 ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kufikia mafanikio hayo.
Chanzo; Mwananchi