James Milner amevunja rekodi ya kucheza mechi nyingi zaidi katika historia ya Ligi Kuu England (EPL), baada ya kuanza katika mchezo wa Brighton dhidi ya Brentford hapo juzi na kufikisha mechi 654.
Milner alibadilishwa katika dakika ya 90 ya ushindi wa Brighton wa mabao 2-0 kule London Magharibi, akipigiwa makofi kutoka kwa mashabiki wa timu zote mbili ndani ya Uwanja wa Gtech.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alikuwa amefikia rekodi ya mechi 653, iliyowekwa na Gareth Barry wa Aston Villa, mapema mwezi huu.
Milner amezichezea kwa nyakati tofauti, Leeds United, Newcastle United, Manchester City, Liverpool na Brighton, akishinda mataji mawili ya Ligi Kuu alipokuwa Etihad na moja Merseyside chini ya Kocha, Jürgen Klopp.
"Kumekuwa na mazungumzo mengi kuhusu hilo. Kwangu mimi, yeyote anayenijua, jambo muhimu zaidi limekuwa timu," alisema Milner akiiambia BBC Radio 5 Live baada ya mchezo huo.
Chanzo: Nipashe