UEFA imethibitisha kuwa ripoti rasmi ya mechi ya jana kati ya SL Benfica na Real Madrid ipo katika hatua ya mapitio.
Kupitia taarifa yao, UEFA imesema kuwa endapo kutabainika masuala yoyote yaliyoripotiwa, taratibu za kinidhamu zitafunguliwa, na iwapo adhabu itaamuliwa, itatangazwa rasmi kupitia tovuti yao ya nidhamu.
Mwamuzi wa mchezo huo, François Letexier, anatarajiwa kuwasilisha ripoti ya mechi, huku Kamati ya Udhibiti, Maadili na Nidhamu ya UEFA ikipanga kuamua iwapo uchunguzi rasmi utafunguliwa.
Kwa mujibu wa mwongozo wa UEFA, mchezaji yeyote atakayebainika kufanya vitendo vya kibaguzi lazima apewe adhabu ya kusimamishwa kucheza kwa angalau mechi 10, sambamba na kushiriki programu maalum ya uhamasishaji na elimu itakayoendeshwa na klabu husika.
Hatua hii inakuja kufuatia madai ya mchezaji wa Benfica, Gianluca Prestianni, kumtolea maneno ya utata nyota wa Real Madrid, Vinícius Júnior, huku akiwa ameziba mdomo kwa jezi yake tukio lililozua mjadala mkubwa mitandaoni na katika ulimwengu wa soka.
UEFA imesisitiza kuwa kwa sasa haina maelezo ya ziada hadi mapitio ya ripoti yatakapokamilika.
Chanzo; Global Publishers