Mashabiki wawili wa klabu ya Chelsea ya England wanaripotiwa kuchomwa visu katika mji wa Naples, Italia, baada ya kudaiwa kufukuzwa na kundi la mashabiki sugu wa Napoli maarufu kama Ultras wapatao 25, siku moja kabla ya timu hizo kukutana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo limetokea jana Jumanne usiku wakati mashabiki hao wa Chelsea walipokuwa wakitembea kuelekea katika baa moja jijini humo. Inadaiwa walivamiwa ghafla na kundi la Ultras waliokuwa na visu, hali iliyoibua hofu kubwa miongoni mwa wageni hao.
Mashabiki wawili walikimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu, huku Chelsea ikithibitisha kuwa majeruhi hao walipata majeraha yasiyo ya kuhatarisha maisha. Baada ya tukio hilo, klabu hiyo imetoa onyo kwa mashabiki wake wote waliopo Naples kuchukua tahadhari kali.
Mmoja wa mashabiki hao alichapisha picha kwenye mitandao ya kijamii akionyesha mkono wake uliokuwa umejaa damu, akidai kuwa alichomwa kisu. Katika ujumbe wake ameandika: “Hakuna mtu atokaye nje Naples leo usiku, hali ni mbaya sana.”
Shahidi mmoja aliyeandika kwenye mtandao wa X amesema walikuwa wanaelekea tu kwenye baa nyingine bila kutafuta ugomvi wowote.
Chanzo; Mwananchi