Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ndege maalum (Boeing 787-8 Dreamliner) kwa ajili ya kwenda nchi Morocco kuwachukua Wachezaji wa Timu ya Kandanda ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ambayo walikuwa wanashiriki mashindano ya AFCON na kuwarejesha jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa amesema Mheshimiwa Rais Samia ametoa ndege ya kuwasafirisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi walioko Morocco wakiongozwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Paul Makonda ikiwa ni kutambua heshima kubwa waliyolijengea Taifa la Tanzania katika mashindano hayo makubwa Barani Afrika licha ya kuondolewa na wenyeji Morocco katika hatua ya 16 ambayo hawakuwahi kuifikia.
Pamoja na kuwatumia ndege ya kuwasafirisha Taifa Stars kutoka Morocco kurejea Tanzania, Mheshimiwa Rais Samia ameandaa hafla ya chakula cha mchana itakayofanyika tarehe 10 Januari 10, 2026 katika Ikulu ya Magogoni Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwapongeza rasmi Taifa Stars pamoja na wanamichezo wengine waliofanya vizuri katika michezo mbalimbali.
Ndege maalum iliyotolewa na Mheshimiwa Rais Samia aina ya Boeing 787-8 Dreamliner inatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam kesho Januari 6, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri na itawasili Jijini Rabat Morocco kesho hiyohiyo majira ya saa 4:30 usiku, kisha itaondoka jijini Rabat Morocco Januari 7, 2026 na kuwasili jijini Dar es Salaam siku hiyo majira ya saa 2:00 usiku katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Chanzo; Itv