Hatuzungumzi soka tunagusa sanaa na kipaji cha upekee cha Michel Kuka Mboladinga, maarufu kama Lumumba au Lumumba Vea. Mmoja wa mashabiki wa kipekee wa soka barani Afrika ambaye huwavutia wengi kwa tabia yake ya kushabikia akiwa amesimama bila kutikisika wakati timu ya taifa lake DR Congo ikicheza katika mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 iliyofanyika nchini Morocco. Mfahamu Zaidi.
Mboladinga alizaliwa Septemba 26,1976 tangu utoto wake alionyesha shauku ya pekee kwenye soka pamoja na kupenda utamaduni na historia ya taifa lake.
Safari yake kama shabiki mwenye ushabiki wa kipekee ilianza mwaka 2013, alipochagua kujitolea kushabikia mechi za timu ya taifa kwa njia isiyo ya kawaida ya kuinua mkono wake wa kulia juu huku akiwa amesimama bila kusogea muda wote wa mchezo ukiwa unaendelea yaani hujifanya kama sanamu.
Kipaji chake hicho cha kipekee kilivutia wengi na kumjengea jina kama shabiki ambaye haoneshi hisia zake wakati mchezo ukiendelea hata pale mpira ukiingia nyavuni. Tabia yake ya kushabikia bila kutikisika ilihusishwa na kumbukumbu ya kisiasa na kihistoria.
Ambapo Mboladinga huiga sanamu ya Patrice Lumumba, kiongozi wa uhuru wa Kongo na waziri mkuu wa kwanza wa taifa hilo baada ya uhuru mwaka 1960, ambaye anaheshimiwa kwa kujitoa kwake kwa taifa hasa kwa kupigania uhuru kwa taifa lake. Ikumbukwe Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961.
Katika mechi kadhaa za AFCON 2025-26, Mboladinga ameendelea kujizolea umaarufu akiwa amevalia nguo zenye rangi za bendera ya DR Congo-bluu, njano na nyekundu.
Chanzo; Mwananchi Scoop