Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Bendera ya Tanzania Kupepea Kriketi Kombe la Dunia

Tanzania imeandika historia mpya katika ramani ya michezo ya dunia baada ya Timu ya Taifa ya Kriketi chini ya miaka 19 kufuzu kwa mara ya kwanza kushiriki Kombe la Dunia la Kriketi, mafanikio yaliyotajwa kuwa ushindi wa taifa zima na ushahidi wa uwekezaji sahihi kwa vijana.

Akizungumza katika hafla ya kuiaga timu hiyo kuelekea mashindano ya Kombe la dunia, Januari 6, 2026 jijini Dar es salaam, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya mipango ya muda mrefu, nidhamu na maandalizi ya kitaalamu yaliyofanywa na Chama cha Kriketi Tanzania kwa kushirikiana na Serikali.

“Hili si tukio dogo, Tanzania imechaguliwa kati ya mataifa 29 ya Afrika kuwa taifa pekee la wanachama wasaidizi lililofuzu. Huu ni ushindi mkubwa kwa taifa letu,” amesema Mhe. Mwinjuma.

Mhe Mwinjuma amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya maendeleo ya michezo kwa kutambua michezo kama chombo cha ajira, afya ya jamii na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Amebainisha kuwa, timu hiyo imeandaliwa chini ya makocha wataalamu, imepata mafunzo ya viwango vya juu, michezo ya majaribio ya kutosha pamoja na mikataba rasmi inayowahakikishia ustawi wao kama wanamichezo wa kulipwa.

Katika hotuba yake, Mhe. Mwinjuma amewataka vijana hao kwenda kuitumikia Tanzania kwa nidhamu, uzalendo na mshikamano, akisisitiza kuwa wao ni mabalozi wa taifa ndani na nje ya uwanja.

“Hamuwakilishi familia zenu pekee, mnaibeba Tanzania nzima. Nidhamu yenu na mwenendo wenu vitaizungumza Tanzania kabla hata ya matokeo ya mechi,” amesema.

Amepongeza uongozi wa Chama cha Kriketi Tanzania chini ya Mwenyekiti wake, Dkt. Sreekumar, akikitaja chama hicho kuwa mfano wa uongozi wa maono, uwazi na uwajibikaji kwa vyama vingine vya michezo nchini.

 

 

Chanzo; Bongo 5

Kuhusiana na mada hii: