Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amewataka wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025, akisisitiza kwamba ushindi mwembamba wa chama hicho unaweza kuleta changamoto katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akihutubia mkutano wa kampeni katika Kata ya Buhongwa, Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, leo Jumanne, Oktoba 7, 2025, Samia amesema ushindi wa 'goigoi' hautaipa Serikali nguvu ya kutosha kuendeleza ajenda za maendeleo kwa kasi inayotarajiwa.
“Tunawaomba tarehe 29 wote waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura watoke wakapige kura. Na unapotoka, usitoke peke yako, utoke na rafiki yako, utoke na familia. Mabalozi hakikisheni nyumba zote wanapiga kura,” amesema. Akiendelea, Samia amesisitiza kuwa kura nyingi za ndiyo kwa CCM zitakuwa ni heshima kwa chama hicho na kwa taifa kwa ujumla.
“Hii ni kukipa heshima chama chetu na kukipa nguvu kikatekeleze yale ambayo tumeyaweka kwenye kitabu. Tukifanya hivyo, yeyote ukimwambia ‘tukopeshe tukajenge barabara’, atasema hiki ni chama pendwa, kimeshinda vizuri- fedha hii hapa, chukueni. Lakini tukishinda goigoi... mambo yatakuwa magumu kidogo,” amesema Samia.
Chanzo: Mwananchi