Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema usimamizi mzuri wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) umewezesha kuondoa wananchi wengi kwenye umaskini.
Akizungumza leo Alhamisi Septemba 18, 2025, mbele ya maelfu ya wananchi wa Zanzibar, Samia amesema ikiwa atachaguliwa tena katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ataendeleza usimamizi wa Tasaf na kutoa mikopo isiyo na riba ili kuimarisha biashara ndogondogo nchini.
“Kule Bara niliahidi kurasimisha biashara ndogondogo, jambo hili ni la Muungano na tutalifanya pamoja pia Zanzibar,” amesema.
Aidha, ametaja mafanikio ya awamu ya sita kuwa ni kukuza diplomasia, kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa na kuongeza heshima ya Tanzania kimataifa. Amesisitiza manufaa ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akisema ndiyo msingi wa ustawi wa Taifa, akirejea maneno ya Mwalimu Nyerere aliyouita Muungano huo ‘Lulu ya Afrika’.
Chanzo; Mwananchi