Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika akizungumza na wanahabari kwenye viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam leo, Jumatano Septemba 10.2025 amefafanua hoja sita (6) zilizowasilishwa na chama hicho kupitia kwa Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu, kuhusiana na kutokubaliana kwao na maombi ya Said Issa Mohamed na wenzake wawili (2) wanaoomba kupatiwa nyaraka kadhaa muhimu za kiofisi za chama hicho.
Ikimbukwe kuwa katika kesi ya msingi inayoendelea Mahakamani hapo, aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar Said Issa Mohamed na wenzake wanadai kuwa chama hicho kimekuwa kikiitenga Zanzibar katika shughuli zake na hakizingatii usawa wa mgawanyo wa mali, raslimali fedha nk.
Sambamba na hilo wanadai kuwa chama hicho kupitia viongozi wake kimekuwa kikitoa kauli zinazoashirikia udini, ukosefu wa usawa wa kijinsia na viashiria vya kuvuruga muungano, jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya CHADEMA, Katiba ya Nchi na Sheria ya Vyama vya Siasa Nchini.
Leo (jana)kesi hiyo inayosikilizwa chini ya Jaji Hamidu Mwanga imetajwa Mahakamani hapo, kwaajili kusikiliza mapingamizi yaliyowekwa na wadai ambapo baada ya kusikiliza hoja za Mawakili wa pande zote mbili, Mahakama sasa inatarajiwa kutoa 'uamuzi mdogo' Juni 29.2025, saa 5 asubuhi, Kufuatia uwepo wa kesi hiyo, kwa sasa CHADEMA imezuiliwa kuendesha shughuli zote za kiitendaji na kisiasa, kutumia raslimali za chama ikiwemo majengo, fedha nk hadi hapo kesi ya msingi, ambayo bado haijaanza kusikilizwa itakapoamuliwa.
Chanzo Bongo 5