Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ametuma salamu za pongezi kwa wananchi wote, wanajeshi wastaafu, pamoja na wanajeshi na watumishi wa kiraia wa Vikosi vya Ulinzi kwa maadhimisho ya Siku ya Walinzi wa Taifa, akieleza kuwa siku hiyo ni ishara ya umoja wa kitaifa.
Katika hotuba yake ya kuadhimisha siku hiyo ya Februari 23, Putin amesisitiza umuhimu wa kihistoria wa maadhimisho hayo, ambayo kwa miongo mingi yamekuwa miongoni mwa sikukuu kuu za kitaifa nchini Urusi. Alisema tarehe hiyo inaakisi heshima na shukrani za dhati za wananchi kwa wale waliotoa maisha yao kulitumikia taifa na kulinda uhuru na usalama wake.
Putin alibainisha kuwa vizazi vingi vya Warusi vimehifadhi kumbukumbu ya historia ya kijeshi ya nchi hiyo, iliyojengwa kupitia umahiri wa makamanda wakuu na ujasiri wa wanajeshi waliojitokeza kuilinda nchi yao kila walipoitwa. Alisema uzalendo na uaminifu wao kwa kiapo cha kijeshi uliweka msingi wa mila na desturi za kijeshi zinazodumu hadi leo.
Rais huyo pia alikumbusha kuwa mwaka 2026 umetangazwa kuwa Mwaka wa Umoja wa Watu wa Urusi, akisisitiza mshikamano wa kihistoria wa makabila na dini mbalimbali nchini humo. Alieleza kuwa katika nyakati zote za historia, watu wa asili na imani tofauti waliungana kuitetea nchi yao kwa ari ya uzalendo na wajibu wa pamoja.
Akirejea operesheni maalum ya kijeshi inayoendelea, Putin alisema wawakilishi wa mataifa yote ya Urusi kwa sasa wanapigana bega kwa bega kulinda maslahi ya taifa, wakiendeleza urithi wa ujasiri na heshima waliouachiwa na mababu zao.
Alisisitiza kuwa uwezo wa kuungana kwa lengo la pamoja umekuwa nguvu kuu ya Jeshi la Urusi na jamii yake ya makabila mengi, akieleza imani yake kuwa hali hiyo itaendelea daima.
Akizungumzia mipango ya baadaye, Putin alithibitisha dhamira ya serikali kuendelea kuimarisha Jeshi na Jeshi la Wanamaji, kwa kuzingatia maendeleo ya kimataifa na uzoefu uliopatikana katika operesheni maalum ya kijeshi. Alisema kipaumbele kitaendelea kuwa kuendeleza nyenzo za kimkakati za nyuklia (nuclear triad) ili kuhakikisha usalama wa Urusi na kudumisha mizania ya nguvu duniani.
Aidha, alibainisha kuwa juhudi zitaongezwa kuboresha utayari wa mapigano, uwezo wa uhamaji na matumizi ya teknolojia za kisasa katika matawi yote ya Vikosi vya Ulinzi, pamoja na kuharakisha maendeleo ya mifumo ya kisasa ya kijeshi.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Putin aliwashukuru wanajeshi wote wa Urusi kwa huduma yao ya kishujaa na kuwatakia heri familia na wapendwa wao.