ACT Walitosa Gari la INEC
Chama cha ACT Wazalendo kimelikataa gari jipya lilitolewa na kwa mgombea wake wa urais, Luhaga Mpina na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (INEC)
Uamuzi huo wa kulikataa gari umetangazwa na Mwanasheria Mkuu wa wa chama hicho, Omar Shaban mara baada ya Mpina kuteuliwa na INEC kuwa mgombea wa urais wa Tanzania na Fatma Fereji kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Tangazo la kupatiwa gari jipya lilitolewa na Mwenyekiti wa INEC jaji mstaafu Jacobs Mwambegele ambaye alisema, “Pamoja na kuwapongeza kwa uteuzi wenu, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inakukabidhi mgombe wa kiti cha rais gari moja jipya aina ya Land Cruiser GX-VXR kwa ajili ya kampeni. Hivyo namuelekeza Mkurugenzi wa Uchaguzi wakati anawasindikiza, akakukabidhi gari hilo pamoja na dereva atakayekuhudumia muda wote wa kampeni asante tunawakia kampeni zenye mafanikio”.
Mara tu baada ya jaji Mwambegele kumaliza kutoa maelezo ya gari, papo hapo akainuka Mwanasheria Mkuu wa ACT, Omar Shaban akasema: Kwanza tunashukuru sana kwa ukarimu ambao tumeelezwa kuhusu kumkabidhi mgombea gari Pamoja na walinzi.
Nimeagizwa na kamati ya uongizu wa chama kushukuru kuhusu jambo hili, lakini pamoja na hayo chama kimenielekeza ni-communicate kuwa kwenye rasilimali ya gari tunashukuru tuko vizuri, tutaomba lisaidie kwa matumizi mengine.
Kwa uamuzi huo ACT Wazalendo kinakuwa chama cha kwanza cha siasa na cha pekee miongoni mwa vyama 18 vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa Tanzania 2025 kulikataa gari jipya la INEC. Wagombea wengine 17 akiwemo Samia Suluhu Hassan wa CCM walikabidhiwa magari mapya Agosti 27, 2025 ambayo ilikuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa nafasi ya urais.
Siku hiyo Mpina na mgombea mwenza Fereji walizuiwa kuingia ofisi za INEC kukabidhi fomu, hivyo ACT na Mpina waliamua kwenda Mahakama Kuu kuupinga uamuzi kwa kumuengua mgombea kwa sababu ya kukosa vigezo.
Alhamisi Septemba 11, jopo la majaji watatu; Abdi Kagomba (kiongozi wa jopo), Evaristo Longopa, na John Kahyoza lilkubaliana na hoja za msingi za walalamikaji dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na INEC, hususan kukiukwa kwa Katiba ya Tanzania, inayotoa uhuru kamili kwa INEC na kuzuiwa kupokea maelekezo kutoka kwa mtu au taasisi yoyote na pia walalamikaji kutopewa fursa ya kusikilizwa. Hivyo jopo hilo likawapa ushindi walalamikaji.
Chanzo; Bbc Swahili