Benki zote nchini Malawi zinatarajiwa kufunga milango yake leo, kama sehemu ya hatua za kuimarisha usalama kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa kitaifa.
Chama cha Mabenki nchini Malawi (BAM) kimebainisha hatua hiyo katika taarifa yake iliyotolewa mapema leo, kikisema hatua hiyo ya tahadhari inafuatia mashauriano na mamlaka husika yenye lengo la kuwalinda wafanyakazi, wateja na miundombinu ya benki katika kipindi hiki.
“Benki zote zitafunga leo mchana ili kuwezesha hatua za usalama kuimarishwa. Tunaomba uelewa na ushirikiano kutoka kwa umma tunapotanguliza usalama wakati huu muhimu,” BAM imesema.
Uamuzi huo unakuja huku kukiwa na wasiwasi mkubwa wa umma wakati taifa linasubiri Tume ya Uchaguzi ya Malawi kutoa matokeo rasmi ya uchaguzi wa Septemba 16, mwaka huu.
Vyombo vya usalama tayari vimeongeza uwepo wao katika miji mikubwa na miji ili kuzuia machafuko yanayoweza kutokea.
Ingawa kufungwa mapema kunaweza kuwasumbua wateja, BAM imesisitiza kuwa hatua hiyo ya muda inaonyesha kujitolea kwake kwa usalama na utulivu wa umma.
Pia imesema huduma za kawaida za benki zinatarajiwa kurejea tena pindi hali ya kiusalama itakapotengemaa.
Chanzo: Nipashe