Mgombea ubunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, ameeleza nia yake ya kuwania nafasi hiyo ya ubunge ni kuwatumikia wananchi wa jiji hilo.
Makonda ameeleza hayo leo, Jumamosi, Septemba 20, 2025, wakati wa maombi katika Huduma ya Radio Safina Mbauda, jijini Arusha.
Huku akitokwa na machozi, Makonda amesema nia yake ya kugombea ubunge ni kutimiza kusudi la Mungu lililopo ndani yake, huku akiomba waumini kumuombea na kujitokeza kupiga kura ili ashinde katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Amesema taifa linahitaji viongozi watakaotimiza kusudi la Mungu hapa duniani, wenye maono na wasiotanguliza maslahi binafsi, ili watekeleze matakwa ya waliowachagua kuwa kwenye mamlaka.
Chanzo; Mwananchi