Hatimaye, Mirambo Yusuf amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Chama cha Wananchi (CUF) baada ya kupata kura 257 alizopigiwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa dharura wa chama hicho, uliofanyika katika Ukumbi wa Lekham, Buguruni, jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Jumapili Februari 22, 2026.
Hata hivyo, mshindani wake aliyefuatia kwa wingi wa kura, Othman Omar Dunga, amepata kura 177 na ameonyesha wasiwasi kwa wajumbe walioshiriki katika uchaguzi huo, akidai kuwa ana mashaka nao kwa kuwa wengi wao hawakuwa wajumbe halali kwa mtazamo wake.
Mirambo, ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Kigoma Mjini, amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa nne wa chama hicho, akirithi rasmi mikoba ya Profesa Ibrahim Lipumba katika nafasi hiyo. Mgombea wa tatu, Nkunyunyika Siwale, alipata kura 6 kati ya jumla ya kura 448 zilizopigwa, huku kura sita zikiharibika.
Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Miraji Mtibwiliko amepata kura 264 na kuwashinda Mohammed Ngulangwa aliyepata kura 88 pamoja na Mussa Mbarouk aliyepata kura 82.
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar imechukuliwa na Haroub Mohamed Shamsi aliyepata kura 256, akimshinda Mbarouk Seif Salim aliyepata kura 171, huku Amina Rashid Salim akijitoa kabla ya upigaji kura.
Chanzo; Mwananchi