Chama cha DP kimemsimamisha uanachama Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Peter Agaton Magisiri ambaye pia ni Mgombea Urais Zanzibar pamoja na wanachama wengine saba kwa tuhuma za kumuunga mkono mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk. Husein Ally Mwinyi.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho ambae pia ni mgombea wa Urais wa Tanzania wa chama hicho, Juma Mluya wakati akizungumza na waandishi wa habari Wilayani Kahama mkoani Shinyanga, baada ya kuahirisha mkutano wake kufuatia kuwa na vikao mbalimbali kwa njia ya mtandao kutokana na kauli za makamu mwenyekiti zenye lengo la kuvuruga msimamo wa chama.
"Hatuwezi kuwavumilia viongozi wasio waadilifu wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti ambae sio msemaji wa chama kwa mujibu wa katiba yetu, Mwenyekiti ndio msemaji ambae ndio mimi, hivyo nimemuagiza Katibu mkuu kuwaandikia barua ya kuwasimamisha uongozi wakiwemo wajumbe na wanachama walioshiriki kwenye kikao hicho" alisema Juma.
Chanzo: Nipashe