Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amesema kuwa hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma kuamuru kuwa Luhaga Mpina ana haki ya kurejesha fomu ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imethibitisha kuwa chama hicho hakifanyi kazi kwa mizaha bali kinafuata kanuni na taratibu za kumpata mgombea urais bora.
Ametoa kauli hiyo mbele ya wanahabari jana Septemba 11, 2025 mara baada ya Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma, kuamuru mwanachama wa ACT Wazalendo, Luhaga Mpina, aruhusiwe kuendelea na mchakato wa kurejesha fomu ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na zuio lililowekwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kumzuia kurejesha fomu na kumnyima nafasi ya kusikilizwa, kuwa kinyume cha sheria na Katiba.
Naye Mgombea Mwenza wa Urais kupitia ACT Wazalendo, Bi. Fatma Fereji, ameipongeza Mahakama kwa uamuzi huo, huku akivishukuru vyombo vya habari kwa kufuatilia kwa karibu mwenendo mzima wa shauri hilo.
Chanzo EATV