Chama cha ACT Wazalendo kimesema kimepokea barua tatu za mapingamizi ya uteuzi dhidi ya Mgombea wa Urais wake Luhaga Joelson Mpina ambapo mapingamizi hayo yamewekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mgombea Urais wa Chama cha AAFP na Mgombea Urais wa Chama cha NRA.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Shangwe Ayo, imenukuliwa ikieleza yafuatayo “hatua hii ambayo Chama kiliitarajia imekuja baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kuiamuru Tume ya Uchaguzi kupokea fomu za Mgombea wetu Ndugu Mpina na kuendelea na hatua za uteuzi wake kwa mujibu wa sheria kutokana na hapo awali ambapo Tume hiyo ilikuwa imemzuia kinyume na sheria kuwasilisha fomu zake za uteuzi”
“Baada ya kupokea na kusoma barua za mapingamizi yaliyowekwa, tumebaini kuwa sura za mapingamizi yote matatu ni madai yasiyo na ukweli wala msingi wowote ya CCM na Serikali yake kupitia kwa Msajili wa Vyama vya siasa kwamba Luhaga Mpina hakuteuliwa kwa mujibu wa taratibu za Chama kuwa Mgombea Urais”
“Wanasheria wa Chama wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Chama Omar Said Shaaban wanajibu mapingamizi yote matatu yaliyowekwa na tutayawasilisha ndani ya muda wa kisheria”
Chanzo: Millard Ayo