Wanahabari duniani kote wametakiwa kutengeneza mpangokazi wa kukabiliana na taarifa potoshi zinazoendelea kusambaa kwa wingi kutokana na ukuaji wa teknolojia.
Hayo yamesemwa na Alexandre Gurreiro kutoka Global Fact Checking Network wakati akizungumza na vijana wanaojihusisha na habari katika Kongamano na Kusanyiko la Vijana Duniani (World Youth Festival Assembly) linalofanyika kwa siku ya tatu mfululizo katika jiji la Niznhy Novgorod nchini Urusi.
Akieleza uzoefu wake katika kukabiliana na upotoshaji kwa kutolea mfano Umoja wa Ulaya, amesema mbinu kubwa ambayo imekuwa inatumika ni kutengeneza habari zinazofanan na ukweli kuhusu watu au nchi zinazotaka kufanyiwa propaganda na kisha kuzisambaza katika vyombo vya habari vinavyomilikiwa na watu hao ili kuzisambaza.
“Zipo kanuni tano za kuhakikisha kama taarifa unayopewa ni potoshi, kwanza kabisa soma ili uelewe na sio uamini, kisha agalia kama kuna haki au uhuru wa mtu unaoporwa ambapo kwa namba tatu fuatilia kama taarifa ina namna yoyote kuna msimamo wa kisiasa unasemwa au kutetewa ambapo kwa namba nne angalia kama kuna vyanzo vya kuaminika vya taarifa hiyo na kisha namba tano kama ni taarifa ya uchunguzi hakikisha dodoso zilizotumika ni zile ambazo hazijaegemea upande mmoja”, amesema Gurreiro.
Katika mioja ya mifano ambayo Gurreiro ameitoa ni namna ambavyo kumekuwa na upotoshaji wa makusudi kuhusu Rais wa Ukraine, Vlodomiry Zelensky ambapo baadhi ya waandishi au vyombo vya habari kwa makusudi vimekuwa vikitetea au kuweka chumvi kwenye masuala yanayomhusu ambapo mfano mmojawapo alitolea kuhusu tuhuma za kufungiwa kwa Chama Cha Kikomunisti nchini humo.
Vijana waliohudhuria majadiliano hayo walipata nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu taarifa potoshi ambapo wengi walieleza changamoto ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo katika kuzitambua taarifa potoshi.
Kongamano la Vijana Duniani linaandaliwa na Shirikisho la Masuala ya Vijana (Rosmolodezh), kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Niznhy Novgorod limeendelea kwa siku yaa tatu likiwakutanisha vijana 2000 toka mataifa mbalimbali likilenga kufungua ushirikiano baina ya vijana duniani kote ambapo mada mbalimbali kuhusu ujasiriamali, ubunifu, vyombo vya habari na masuala ya kijamii vimeendelea kuwa sehemu kubwa ya mjadala.