Ripoti zinaeleza kuwa Apple inapanga kuingiza teknolojia ya Samsung kwenye mfumo wa sensa za kamera za iPhone kuanzia takribani mwaka 2026 hatua itakayomaliza enzi ndefu ya Sony kuwa msambazaji pekee wa sensa za kamera za iPhone.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa Apple inavutiwa na muundo wa sensa wa tabaka tatu (three-layer stacked design) unaojulikana kama PD-TR-Logic unaolenga kusafirisha data ya picha kwa kasi zaidi na kwa ubora wa juu kwenda kwenye mfumo wa uchakataji wa picha wa Apple.
Teknolojia hiyo inatarajiwa kuboresha kasi, usahihi na ubora wa picha kwa ujumla.
Kwa kampuni kubwa kama Apple, kutumia wasambazaji zaidi ya mmoja (dual sourcing) ni mkakati wa kimkakati unaosaidia kupunguza hatari za uzalishaji hasa wakati mahitaji ya soko yanapoongezeka kwa kasi wakati wa uzinduzi wa bidhaa mpya.
Endapo Samsung itaingia rasmi kwenye mnyororo wa usambazaji, simulizi ya kamera ya iPhone haitahusu tu ubora wa picha bali pia mkakati wa ugavi na ushindani wa kiteknolojia kati ya magwiji hawa wawili wa teknolojia.
Chanzo; Bongo 5