Mapema Januari 2026, kumetokea jambo kubwa kwenye Instagram! Idadi kubwa ya watu wanasema kuwa taarifa za watumiaji zaidi ya milioni 17.5 zimevujishwa. Ambapo data hizi zinajumuisha majina ya watumiaji (usernames), namba za simu, barua pepe, hata anwani za nyumbani kwa baadhi yao. Habari hizi zimeanza kuuzwa au tolewa bure kwenye mitandao ya giza (dark web) tangu tarehe 7 Januari 2026.
Baada ya data hizo kuvujika, wavamizi wameanza kufanya vitendo vya ujanja. Wengi wenu mmeshapokea barua pepe nyingi sana kutoka Instagram zinazokuambia "Reset password yako sasa!" au "Mtu anajaribu kuingia kwenye akaunti yako!" Hizo barua pepe zinaweza kuwa za kweli (Instagram wenyewe wanakubali kuwa kuna tatizo lililosababisha reset nyingi), lakini wengi wao ni mtego wa wizi!
Wavamizi wanatumia taarifa zako ili kuomba reset ya password yako mara kwa mara. Kama mkiwa mna bahati mbaya na mkibonyeza link iliyomo kwenye barua pepe hiyo, wanaweza kuiba akaunti yenu kabisa.
Instagram (Meta) wamesema "Hakuna uvamizi wa mfumo wetu. Akaunti zenu ziko salama. Tatizo lilikuwa la nje tu, tumelishughulikia. Barua pepe hizo za reset msizifanyie kitu – zipuuze tu. Samahani kwa usumbufu."
Lakini wataalamu wa usalama wa mtandao wanasema:
Hata kama hakuna "breach" ya moja kwa moja kwenye Instagram, data hii iliyovujika inaweza kuwafanya wavamizi kuwashambulia watu kwa urahisi zaidi. Wanaweza kutuma barua pepe za uongo zinazoiga za Instagram, au hata kujaribu kudanganya ili wapate password yenu.
Ushauri wa haraka kwa Watanzania wote wanaotumia Instagram:
- Weka two-factor authentication (2FA) mara moja – tumia app (kama Google Authenticator) badala ya SMS.
- Usibonyeze link yoyote kwenye barua pepe ya "reset password" isipokuwa ukiingia Instagram moja kwa moja kupitia app au www.instagram.com.
- Badilisha password yako iwe ngumu(mchanganyiko wa herufi kubwa, ndogo, namba na alama).
- Kama umepokea barua nyingi za reset bila kutarajia – angalia akaunti yako mara moja, angalia "Login Activity" na "Connected Devices" kwenye settings.
- Jihadharini sana wiki hizi – wizi wa akaunti umeongezeka sana!
Chanzo; Tanzania Journal